Jaja ni hatareee!

♠ Posted by Unknown at 12:19
 
Genilson Santos Santana ‘Jaja’
INAWEZEKANA hii ndiyo habari ambayo mashabiki, wadau na viongozi wa Yanga wanahitaji kuisikia, Yanga imeifunga Chipukizi ya Zanzibar bao 1-0, lakini habari nzuri ni kuwa Genilson Santos Santana ‘Jaja’ na Andrey Coutinho walikuwa ni habari
nyingine uwanjani.
Wachezaji hao wa Yanga, raia wa Brazil ambao walicheza kwa dakika 45 katika mechi hiyo ya kirafiki kwenye Uwanja wa Gombani, jana, walionyesha uwezo mzuri ambapo Jaja ndiye alikuwa mfungaji wa bao pekee kwa kichwa.
Jaja alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kupata krosi nzuri ya kiungo Haruna Niyonzima ambaye alitua klabuni hapo wiki iliyopita, tofauti na wachezaji wenzake waliofika mapema, sababu kubwa ikiwa ni kuitumikia timu ya taifa ya Rwanda.
Niyonzima ambaye alionekana kupiga pasi nyingi za kueleweka, alinogesha mchezo huo na kuonekana kuelewana na wenzake, lakini makali ya Coutinho ndiyo yalikuwa hatari, kwani alionyesha uwezo mkubwa na kuwa staa wa mechi hiyo.
Kutokana na ukali wake aliokuwa akiuonyesha, Coutinho alijikuta akichezewa rafu mara kwa mara na mabeki wa Chipukizi, timu ambayo imeshuka daraja hivi karibuni kutoka Ligi Kuu ya Zanzibar.
Katika mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo, alichezesha vikosi viwili katika kila kipindi lakini kile ambacho kilianza ndicho kilichoonyesha uhai zaidi.
Mara baada ya mchezo huo, Maximo alisema: “Timu bado haijakaa sawa, kuna vitu vya kurekebisha hasa kwenye umaliziaji, vyote tunaendelea kuvifanyia kazi.”
Kikosi cha Yanga kilichoanza kwenye mechi hiyo ni; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Coutinho, Niyonzima, Mrisho Ngassa na Jaja.
Kilichoanza kipindi cha pili ni: Juma Kaseja, Salum Telela, Edward Charles, Rajab Zahir, Said Juma, Omega Seme, Simon Msuva, Nizar Khalfan, Said Bahanuzi, Jerry Kiiza na Hamis Kiiza

                                                Posted by Mr.Prime on August 22, 2014

0 comments:

Chapisha Maoni